This post is also available in:
Martha Lukasi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sibusiso kilichopo jijini Arusha, Tanzania. Mnamo mwaka 2026, kituo hicho kinatarajiwa kuimarishwa zaidi ili kuwa kituo kinachoongoza katika huduma za ukarabati, huku shughuli za uhamasishaji na utoaji huduma zikipanuliwa kupitia mkakati wa Maendeleo Jumuishi ya Kijamii (CBID) unaotumia kliniki zinazohamishika kufikia jamii zilizo mbali. Katika maelezo yake, Martha anaeleza kuhusu mwelekeo huu mpya na shughuli zitakazoongeza upatikanaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum na familia zao.
Martha, Sibusiso imekuwapo kwa miaka 25. Kwa nini sasa kuna haja ya kuwa na mbinu mpya ?
Kwa miaka 25, Sibusiso imekuwa ikitoa huduma za ukarabati kupitia programu zinazotekelezwa katika kituo na kupitia uhamasishaji unaofanyika katika vijiji vilivyo karibu na kituo hicho. Hata hivyo, uzoefu wetu umebaini kuwa mbinu hii pekee haikidhi kikamilifu mahitaji ya familia zinazoishi maeneo ya mbali, zisizo na uwezo wa usafiri, au zinazokumbana na changamoto za unyanyapaa, hali inayowazuia kupata huduma stahiki kwa wakati. Kwa kuzingatia hali hiyo, tumeazimia kuboresha na kupanua mbinu zetu za utoaji huduma ili kuhakikisha kuwa watoto wote, bila kujali mahali walipo, wanafikiwa na huduma za ukarabati kwa usawa na kwa wakati unaofaa.
Sibusiso itafanya nini tofauti sasa?
Mnamo mwaka 2026, Sibusiso itatekeleza mfumo mseto unaochanganya huduma za kituoni na Maendeleo Jumuishi ya Kijamii (CBID), kwa kutoa huduma za ukarabati za kila mwezi kupitia kliniki zinazohamishika. Huduma hizi zitatolewa kwa ushirikiano na jamii, familia, pamoja na mamlaka za serikali za mitaa. Kupitia mbinu hii, tunatarajia pia kupunguza unyanyapaa na kukabiliana na changamoto za kutengwa kwa watoto wenye ulemavu. Mpango huu utaanza kwa majaribio katika kitongoji cha Maji ya Chai, Wilaya ya Arumeru.
Nini kinatokea katika kliniki inayohamishika?
Timu yetu ya wataalamu, wakiwemo wataalamu wa tiba, wafanyakazi wa kijamii na walimu, husafiri hadi maeneo yenye kipato cha chini ili kuwafanyia watoto tathmini, kutoa huduma za ukarabati, kuwajengea uwezo walezi, na kuielimisha familia namna bora ya kuwasaidia watoto wao nyumbani. Aidha, tunashirikiana na watoa huduma za afya wa maeneo husika katika utoaji wa huduma hizi na kuziunganisha familia na huduma zetu za ukarabati. Kupitia mbinu hii, tunalenga pia kuimarisha uelewa kuhusu haki na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika jamii.
Kwa nini ushiriki huo wa jamii ni muhimu sana?
Kwa kuwa mabadiliko ya kudumu hayawezi kutokea yenyewe, bali huanza na jamii yenyewe. Tunapoiwezesha familia, kuelimisha jamii, na kuimarisha ushiriki wa serikali za mitaa, tunapanua fursa kwa watoto wenye ulemavu kushiriki kikamilifu na kunufaika na huduma. Ushiriki wa jamii ni msingi muhimu katika kuondoa unyanyapaa na dhana potofu, kuboresha upatikanaji wa huduma, na kuhakikisha kuwa ujumuishaji unakuwa endelevu na wenye matokeo ya muda mrefu.
Je, mbinu hii ni mbadala wa huduma za ukarabati zitolewazo kituo?
Hapana, kabisa. Kituo chetu kinaendelea kubaki kuwa kitovu cha kazi zetu. Kwa hakika, tunakiimarisha zaidi kama kituo kinachotoa huduma za ukarabati za hali ya juu, sehemu ya kujifunzia, na kituo cha rufaa kwa huduma maalum. Mabadiliko yaliyopo ni kupanua wigo wa huduma ili kuhakikisha kuwa msaada hauishii kituoni, bali unaendelea kuwafikia watoto na familia zao nyumbani na ndani ya jamii.
Hatua hii ina maana gani kwa mustakabali wa Sibusiso?
Hii ni hatua muhimu kuelekea kufikia lengo letu la kuleta athari endelevu na kuimarisha uwajibikaji wa pamoja ndani ya jamii. Lengo letu ni kuwafikia na kuwahudumia zaidi ya watoto na vijana 2,500 wenye changamoto za ukuaji kupitia huduma zetu za ukarabati ifikapo mwaka 2030. Kupitia mbinu hii, watoto wengi zaidi wenye ulemavu wataweza kupata huduma stahiki na fursa bora za kushiriki kikamilifu katika jamii nchini Tanzania.
Je, kuna mabadiliko mengine yoyote kwenye programu za Sibusiso mwaka huu?
Hakika. Kwa kuanza kwa shughuli hizi mpya, tunapitia upya bajeti yetu na kurahisisha upangaji wa programu ndani ya kituo. Kwa mfano, tumepunguza muda wa programu kutoka wiki 7 hadi wiki 4 ili kuwezesha mizunguko zaidi ya huduma kwa mwaka. Aidha, tunaweka msisitizo mkubwa zaidi katika ushiriki wa jamii, kuongeza uelewa, na utetezi wa haki za watoto wenye ulemavu. Tunatekeleza haya kwa kushirikiana kwa karibu na serikali pamoja na jamii za wenyeji ili kuhakikisha uendelevu na matokeo yenye tija.
Hatimaye: ni nini kinachokusukuma wewe binafsi katika mradi huu?
“Kila siku naona tofauti mtoto anapoonekana, kuthaminiwa, na kupewa nafasi ya kustawi. Ninapomwona mtoto ambaye hapo awali alitengwa na sasa anaweza kushiriki, kujifunza, na kukubalika katika jamii yake, inanipa nguvu na matumaini makubwa.”